Tuesday, August 24, 2010

BI ZAINABU SHAHIDI - (sehemu ya kwanza)

BI ZAINABU SHAHIDI - (sehemu ya kwanza)




Nilikuwa najipitia tu asubuhi pale makutano ya mtaa wa Swahili na Mafia; saa moja asubuhi naelekea kazini mitaa ya Samora. Nilikuwa natoka Buguruni kwa mabasi yaendayo Muhimbili nikiwa nimeshukia kituo cha Msimbazi.





Siku hiyo niliamka na nguvu maana mfukoni nilikuwa na kama shilingi laki tatu hivi; ni mara chache kwangu kuamka hivyo na nina imani kwa watu wengi wa aina yangu katika jiji hili pia siyo kawaida hata kwao.



Katika makutano hayo upande wa kulia huwa kuna akina mama wengi sana wamejipanga mstari wameketi na vyombo vyao vya makulaji wakiuza kujitafutia riziki. Mahali hapa kila aina ya kitafunio kinachopatikana nchi hii uliweza kukipata, na pia kila aina ya supu isipokuwa moja tu ile ya Iringa; zote zilikuwa zikipatikana.



Siku hiyo mwenyewe nilishapita kona hiyo lakini kama vipi vile kitu kikaniambia ebu angalia nyuma....hapo ndipo nilipoona hicho nilichokiona.



Sijaelewa ni kwa nini jicho langu moja kwa moja lilifika kwake lakini hivyo ndivyo ilivyotokea.



Alikuwa ni Dada wa miaka kati ya ishirini na tano na therathini. Japo alikuwa ni dada wa kawaida lakini kwa kweli alikuwa mzuri. Kwangu mimi hilo la uzuri halikuwa sana lakini nadhani kuna kitu ambacho kilinigusa zaidi kuhusiana na huyo dada.



Pale mbele yake alipokaa palikuwa na sufuria saizi ya kati limefunikwa likiwa juu ya ndoo. mwenyewe alikuwa kajitanda au sijui kama ni kuvaa ushungi wa rangi ya zambarau na gauni la maua ya kijani na samawati. Nilisimama pale nilipokuwa nimefika na kuendelea kumtazama vizuri ili niweze kukiona kitu ambacho kilinifanya niendelee kumwangalia yeye na si mwingine kati ya kundi zima lililokuwepo mahali pale. Zilipita takribani dakika kumi nzima bila kuona chochote. Nilikuwa kama nimepigwa na bumbuazi hadi nilipokuja kugutuliwa na teja mmoja kwa kunikumbusha kuwa nilikuwa nimesimama barabarani na kwa kipindi ambacho nimesimama pale nilikuwa nimekoswakoswa kugongwa na magari matatu.



Pamoja na masaada wa teja, kilichoweza kinirudia ilikuwa ni fahamu lakini uamuzi wa kuondoka pale nilikuwa bado sijaufikia.



Idadi kubwa ya akina mama pale walikuwa hawajajua kinachoendelea, kama ujuavyo biashara ni asubuhi kila mmoja alikuwa na hamsini zake, hata yule bibie niliyekuwa namwangalia, kwa dakika tano za awali alikuwa hajajua kuwa namwangalia japo baadae aliniona na kubaki akinishangaa.



Sijui kama ni kwa kukerwa au kwa huruma, dada yule aliinuka pale alipokuwa na kunifuata niliposimama akaniuliza kama nilikuwa na mfananisha na mtu ama kulikoni. Kwa hapo sikuwa na jibu zaidi ya kumwuliza kama ulikuwepo uwezekano wa mimi na yeye kukutana mahali mbali na sehemu ile tuweze kuongea zaidi. Ilikuwa kama alikuwa anategemea nitasema vile; alinishauri tukutane Concord Hotel saa saba na nusu mchana na akasisitiza niende na muda kwani hatanisubiri zaidi ya robo saa. Sikusema chochote zaidi ya kuitikia kwa kichwa na kuondoka.



Wakati tayari nimekwisha fika ofisini, ndipo nilipokumbuka kuwa nimefanya makosa mengi sana ya kiufundi. Yule dada sikumwuliza jina na wala sikumwomba namba yake ya simu wala kumpa yangu; hiyo kitu sikuipenda japo nilijipa moyo kuwa makosa kama hayo ni ya kawaida kama ambavyo Ronaldo ama Drogba anavyoweza kukosa panati katika mechi muhimu.



Ikiwa imebaki nusu saa kufikia saa saba na nusu niende kukutana na dada niliitwa ofisini na bosi kutoa taarifa juu ya safari ambayo nilikuwa ninerejea siku mbili zilizopita. Nilijua pengine dakika kumi zingelitosha kuwasilisha taarifa ile kwa kuzingatia kuwa nilikuwa nimeiandika; lakini mambo yalikuwa sivyo hadi inafika saa saba na dakika ishirini bado bosi alikuwa anaendelea kuungurumisha maswali.



Kwa kuona sasa ipo hali ya hatari ya kuikosa ahadi nilimwomba bosi nikajisaidie kwani nilikuwa najisikia tumboni mambo si shwari; alipokubali tu nilichomoka kama chizi na kutokomea mtaani badala ya kwenda uani palepale ofisini. Niliamua nifanye vile kama kutakuwa na hoja basi ni hapo baadae ili mradi nimetimiza ahadi.



Kwa kuona muda ulikuwa umeyoyoma niliamua nichukua teksi inikimbize kwani toka mtaa wa Samora hadi ilipo hoteli ya Concord kulikuwa na umbali. Lakini kama wasemavyo wahenga kuwa ngombe wa maskini hazai na akizaa anazaa dume na dume lenyewe linakufa; hivyo ndivyo ilivyonitokea. Pamoja na jitihada zote za kutaka kuwahi, nilifika Concord Hotel saa nane kasoro dakika kumi. Sikusubiri gari lisimame kwani tayari tulikuwa tumekwisha lipana na dereva. Nilichomoka na kuingia fosi mapokezi kuulizia kama kuna mgeni yeyote yupo hapo anamsubiri mtu; dada wa mapokezi akanifahamisha kuwa alikuwepo dada mmoja ambaye alikuwa amekaa kwa karibu nusu saa hivi lakini muda si mrefu ameondoka kwa gari aina ya Range Rover.



Mwanzoni sikukubaliana na mtu wa mapokezi kuwa anayemsema ndiye niliyemfuata lakini baada ya kupata maelezo ya kina kuwa yule dada alipokuwa akiondoka pale alisema kwa kuwa mwanaume aliyekuwa ameahidiana wakutane pale saa saba na nusu alikuwa amechelewa basi yeye anaondoka. Ama kwa hakika baada ya kupata habari ile nguvu ziliniishia.





*******************

No comments:

Post a Comment