Thursday, October 28, 2010

VITUKO MITAANI

Kuna dada mmoja hajaolewa anakaa nyumba ya kupanga pamoja na wengine ambao wameolewa. Dada huyu alikuwa na tabia ya kila wakati kwenda kuoga akiwa amevaa taulo tu. Kitu hiki hakikuwapendeza wenzake ambao wameolewa kwa kumwona kama anawatega waume zao.




Siku moja wenzake wakapanga njama za kumkomesha. Wakamtafuta mtoto wa mitaani na kumuagiza amvizie anapokwenda kuoga amnyang'anye taulo akimbie nalo. Kwa bahati wakati wanapanga njama hizo dada mhusika alikuwa amejibanza kwenye chumba chake anawasikiliza.



Siku ikafika ya utekelezaji wa njama hizo. Yule dada kama kawaida yake na bila wasiwasi akavaa taulo lake bila kitu kingine kwa ndani na kuelekea kuoga kwenye bafu la nje.



Ghafla akiwa katikati ya nyumba na bafuni yule kijana akatokea na kupora taulo akakimbia nalo. Kipindi hicho karibia wapangaji wote walikuwa hawakucheza mbali wapo jirani jirani kushuhudia matokeo ya mpango wao.



Kinyume cha matarajio yao, yule dada baada ya kuporwa taulo hakustuka hata kidogo kana kwamba hakuna kilichotokea. Akaendelea na safari yake bafuni akiwa mtupu. Baada aya kumaliza kuoga, akatoka bafuni na kuelekea vyumbani kama alivyozaliwa.



Wapangaji wenzake ikabidi wapeleke mashtaka kwa mjumbe na yule dada akaitwa ajieleze kisa cha kuwamwagia radhi wenzake.



Alichosema yule dada, nanukuu "......nashukuru mjumbe kwa kunipa nafasi ya kuongea......kabla ya yote naomba nikukabidhi mchango wangu wa shs 20,000/= ili akaongezewe yule mtoto aliyepewa pesa na wapangaji wenzangu aje anipore taulo wakati ninakwenda kuoga........pili, sioni kwa nini tumeitana kwa sababu kila mtu anajua kuwa matokeo ya kuvuliwa nguo ni kubakizwa uchi, na mimi kwa kulijua hilo nikadhani pengine wenzengu wangependa kuniona nikiwa sina taulo......vinginevyo wasingelimkodi mtu aninyang'anye taulo akimbie nalo kwani wao walitarajia iweje......kwa ujumla mjumbe kama kunatafutwa mkosaji basi ni hawa wenzangu......na kama tunataka kutenda haki.....hawa ndio wanilipe mimi fidia kwa kunidhalilisha kwani taulo sikujivua mwenyewe"



Mjumbe akabaki mdomo wazi.

1 comment: