Saturday, August 14, 2010

TONE LA HUBA

TONE LA HUBA




Nilikuwa nimepanga mtaa wa Majani kwenye nyumba ya Mzee Mbinde; nyumba iliyokuwa na vyumba kumi na viwili vilivyojengwa kwa safu mbili zinazitazamana.



Chumba changu kilikuwa ni cha mwisho kulia ambacho mlango wake ulikuwa ukitazamana na mlango wa chumba cha Seme.



Seme alikuwa ni mvulana mwenye umbile la kadiri kwa kila namna; yaani mfupi kiasi mwembamba kiasi, mweupe kiasi ili mradi kwa ninavyovijua ilikuwa ni kiasi kiasi kiasi.



Mimi mtaa mzima walikuwa wamezoea kuniita Mammy lakini jina langu kamili ninaitwa Mamamia.



Katika nyumba hiyo ya Mzee Mbinde, mimi ndiye nilianza kupanga kabla ya Seme ambaye alihamia hapo baada ya miaka miwili.



Wapangaji wenzetu na majirani wengi hawakumpenda Seme kutokana na mambo yake hayo ya kiasi kiasi; wengi walimwona msiri, mwenye maringo na roho mbaya tofauti na mimi ambaye kwa hakika nilimwona kama kipande dha almasi katika chupa ya kioo isiyofunguka kirahisi.



Tangu ahamie pale nilikuwa nikijitahidi sana kutafuta fulsa ya kuongea nae lakini daima alikuwa na salamu za kiasi na majibu ya kiasi; kiasi kwamba kama si mapenzi ya dhati juu yake na mimi ningeliungana na majirani kumwona si chochote.



Kwa kweli Seme alikuwa ni mvulana wa aina yake. Sikupata kujua anakula saa ngapi, wapi na anakula nini. Sikuwahi kumfahamu rafiki yake, ndugu yake, kabila yake wala dini yake. Seme alikuwa ni ingia toka, sikuijua shughuli yake wala aendako na ashindako muda wote.



Kwa miaka yote nilikuwa ninasumbuka na ninataabika kwa subira kwa imani kuwa ipo siku milango ya Seme itafunguka ili niweze kuupenyeza moyo wangu lakini kinyume na matarajio kila siku iliyokuja ilikuwa ni aheri ya siku iliyopita. Moyo wangu ulizidi kujazwa kutu ana mwenendo wa mwanaume huyu.



Kunako siku ya siku mimi sikulala nilikesha nikiwaza. Hivi ni kwa nini nipate shida hii na huyu anayenipa matatizo yote haya ni nani hasa; ndipo siku hiyo nikapitisha maamuzi kuwa haiwezekani, lazima nimjue huyu Seme kwa undani na baada ya hapo ni nipitishe azimio la mwisho.



Siku hiyo niliamka mapema, nikaoga na kuvaa suruali nzito nyeusi na fulana nyeusi tayari kwa kazi ya ukachero ambayo sikuijua itaishaje. Kwa hofu ya kazi hiyo nikachukua kiasi cha shilingi laki nane ambazo nilikuwa ninazihifadhi nyumbani nikazitia katika mkoba wangu mdogo mweusi. Kwa tahadhari zaidi, nikachukua kitambulisho changu cha kazi, pasi ya kusafiria na kitambulisho cha mpiga kura.



Wakati nakamilisha kufanya vyote hivyo nikasikia mlango wa Seme ukifunguliwa nikajua sasa kazi inaanza.



Nilimwacha kwanza Seme atangulie kidogo, ndipo nilipofunga mlango wa chumba changu na kuanza kumfuata Seme. Seme bila ya wasiwasi wowote alitembea bila ya kugeuka nyuma, na mimi nikawa namfuata bila ya kugeuka nyuma kwa kuhofia kuwa ninaweza wakati mimi nimegeuka, Seme nae akageuka na kuniona bila mimi kujua.



Seme alikata mitaa miwili, kisha akaenda panapo teksi moja ya kukodi. Hapo sasa jasho lilianza kunitoka, lakini nikasema sikubali ni mimi na yeye leo.



Wakati teksi yake inaondoka na mimi tayari nilikuwa katika teksi namwelekeza dereva aifuate teksi iliyokuwa ikiondoka mbele yetu.



Safari ya kufukuzana na Seme ilianza kwa kutumia magari ambayo si yetu na hatukuwa na mamlaka nayo.



Teksi ya Seme ilikuwa ikiendeshwa kasi kuelekea nje ya jiji. Dareva wangu nae alikuwa akijitahidi sana kuifukuzia teksi hiyo lakini kwa tahadhari ya kutoonekana na kutopata ajali japo usoni nilimwona mwenye mashaka.



Nilimtia moyo aendeshe kwani fedha siyo tatizo.



Kwa mbele yetu akina Seme waliingia kituo cha mafuta na hapo nikamwona na dareva wangu akipumua kwa furaha, kumbe shaka yake ilikuwa ni kuishiwa mafuta wakati ukimfukuzia mtu. Tulipunguza mwendo na kuwaacha wajaze na sisi tujaze.



Baada ya shughuli hiyo kazi ya kufukuzana iliendelea.



Sikuamini macho yangu tukiwa katikati ya pori gari ya mbele yetu iliposimama na kumshusha Seme. Kwanza nilipigwa na butwaa kabla sijatoa maelekezo kwa dareva wa teksi niliyoikodi aegeshe gari kwa pembeni nishuke kisha afanya kama anapita akageuzia mbele aje asimame pale niliposhukia.



Nikimlipa pesa yake kwanza haraka haraka na kumwomba namba ya simu endapo nitamhitaji nitampigia.



Nilianza kunyatia kwa nyuma kufuata Seme. Seme alikuwa akiyoyoma ndani ya msitu kama hana akili nzuri. Kama kawaida yake alikuwa hatazami nyuma. Tuliupita msitu, tukaikuta mbuga baadae tukaanza kuiona bahari. Moyo ulianza kunidunda kwa kasi kwa hofu ya huko anakoelekea Seme; lakini kwa kuwa maji ukiyavulia nguo ni lazima uyakoge niliendelea na msafara hadi nikamwona Seme amesimama kando ya bahati.



Hapo aliposimama seme ndipo nilipoanza kuyaona maajabu, nikamwona Seme anainama na kufungua kitu kama mlango chini na kuanza kushuka kitu kama ngazi. Baada ya Seme kupotea na mimi nikaenda eneo hilo hilo, mwanzoni sikuuona mlango huo lakini baadae nikauona. Namimi nikainama na kuufungua, ni kweli nilikuta kuna ngazi zinashuka chini.



Bila ya kuwa na uhakika na ninalolifanya nilitelemka kwa kasi hadi katika chumba ambacho ama kwa hakika tangu nizaliwe sijapata kuona chumba kizuri kama kile. Kwa kuwa hakukuwa na kunakoendelea na Seme simwoni na wala sioni mlango mwingine zaidi ya nilioingilia nikaamua nikae kwenye viti vizuri vya chumba hicho nisubiri kiama changu.



Nilikaa kwa karibu nusu saa nzima lakini sikumwona Seme wala kusikia mlio wowote. Niliendelea kukaa vilevile hadi usingizi uliponipitia.



Nadhani nililala kwa muda mrefu sana hadi jioni nilipoamshwa na Seme lakini tofauti na ilivyokuwa niliamka nikiwa chumbani tena kitandani kwa Seme na Seme mwenyewe amesimama akiniangalia kwa mshangao..."..Mammy umeingiaje chumbani kwangu wakati ufunguo ninao mwenyewe !"



Mpaka hapo sikuwa naelewa kama yanayotokea ni kweli ama ninaota.